Kauli ya wanawake wa Kiafrika ambao wanataka kuwepo kwa haki na ukombozi wa wanawake kuhusu urejeshaji wa uchumi wa Afrika baada ya COVID-19

Utangulizi: Wanawake wa Kiafrika wenye shauku ya kuona kuwepo kwa haki na ukombozi wa wanawake wa Kiafrika wamekusanyika ili kufikiria mustakabali wa uchumi wa kisiasa wa Afrika. Kauli hii kwa wajumbe wa Jumuiya ya Afrika, ambao waliteuliwa kuhamasisha msaada wa kimataifa kwa kufufua uchumi wetu, ina mapendekezo na inawataka wajumbe wajiunge nasi kufikiria upya maendeleo yetu ya kiuchumi. Ikiwa unajitambua kama mwanamke wa Kiafrika mwenye shauku ya kuona kuwepo kwa haki na ukombozi wa wanawake na unakubaliana na mapendekezo tungependa utie sahihi kwenye kauli hii.

Wapendwa Dr Ngozi Okonjo-Iweala, Dk.Donald Kaberuka, Bwana Tidjane Thiam, Bwana Trevor Manuel na Bwana Benkhalfa Abderrahmane, 

Tunawaandikia barua hii kwa nyadhifa zenu kama Wajumbe Maalum ambao Umoja wa Afrika umeamuru kuhamasisha msaada wa kimataifa kushughulikia janga la coronavirus barani Afrika. Sisi ni kikundi cha wanawake wenye shauku ya kuona kuwepo kwa haki na ukombozi ya wanawake wa kiafrika na ambao wamejikita katika maono ya  Afrika iliyokombolewa. Maono haya yanatuwezesha kuthubutu kuamini kwamba kuna suluhisho na rasilimali nyingi yanayoweza kutatua magonjwa mengi ambayo bara letu linakabili. Tunatoka jamii, sekta na nidhamu mbalimbali zikiwemo sheria, haki za wanawake, uhamasishaji wa fedha, uchumi, haki za kilimo na ardhi, afya, uzalishaji wa kitamaduni, masomo ya maendeleo, uhuru wa chakula, haki za ushuru, kazi ya ikolojia na mengineo.

Tunahitaji suluhisho na COVID-19 imetupatia fursa nzuri ya kufikiria upya uchumi wa kisiasa wa Kiafrika. Wakati huu unahitaji majibu ya Kiafrika ambayo yanaunda mazingira ya kuwezesha watu na harakati zao kuongoza kazi ya kiuchumi, zikiwemo uchumi wa vyama vya ushirika na uchumi wa mshikamano, wapewe msaada na nafasi ya kustawi. COVID-19 inahitaji kuwa mahali pa mageuzi kutoka kwa mifano ya uchumi huru na nchi yaliyofadhiliwa zaidi. Mgogoro huu ni fursa ya kuondoa ukosefu wa usawa wa kimuundo na kuweka upya uchumi wa kisiasa. Tumekuwa tukifanya kazi kutengeneza data na kujenga harakati za msingi tangu Mipango ya Marekebisho ya Kimuundo. Wengi wetu – kama wewe – tuliishi kupitia Mpango wa Marekebisho ya Kimuundo na tumejionea nchi tulizobaki nazo. Mgogoro wa kifedha wa 2008 ulikuwa mlipuko wa utandawazi na ukumbusho kwamba masoko ambayo hayana mipaka hayawezi kuwa msingi wa utajiri na usawa. Licha ya nchi zetu kuwa na upungufu moja au nyingine, bado yanabakia kuwa mataifa tunapoishi, tunapozalisha mazao, tunapokula, na tutakapozikwa hatimaye

Mgogoro wa mkopo ulikuwa mkubwa na ulioenea, na ulibadilisha ulimwengu wetu kwa njia ambazo bado tunaendelea kutambua. Cha kusikitisha ni kwamba kuna wakati shida inaweza kosa kusisimua hamu, au hata isionekane. Watu huja kukubali mabadiliko yaliyoletwa na shida. Hii haiwezi kuwa kisa hapa. Uimara wa mantiki ya soko imeshikilia masoko kwa kiwango ambayo imewezesha mifumo ya kiuchumi za kila siku na uzalishaji wa neo-liberal kuonekana sio kama bahati mbaya za utandawazi bali mpangilio wa asili ya ulimwengu wetu. COVID-19 imebomoa ulimwengu huo na tunayo nafasi ya kurekebisha uwezo wa serikali na hatua za kikatili ambazo hutumika mara kwa mara kutekeleza mpangilio wa kijamii kwa wakati kama huu. Miradi kama Mkataba wa Kiafrika ya Ushiriki Maarufu kwa Maendeleo, Ajenda mpya ya Maendeleo ya Afrika 2020, Ushirikiano Mpya wa Maendeleo ya Afrika (NEPAD) haijatoa faida kubwa. Ikiwa jumla ya mipango hii yote ya zamani imetufikisha tulipo kwa wakati huu, tunahitaji kufikiria tena chaguo letu. Tunahitaji mwelekeo wa kina wa maendeleo ya Kiafrika ambayo inaangazia wakati huu na pia baada ya COVID-19.

Wakati Afrika sasa inaelekea kuongeza msaada wa kifedha ili kupunguza athari za janga hili, udhaifu wa sera na mifumo ya ufadhili wa maendeleo haifai kuathiri uhuru wa nchi za Kiafrika au wajibu wao kwa watu wa Afrika. “Ukuaji” wa Kiafrika katika miaka ishirini iliyopita umeambatana na ukosefu wa ajira ulioenea, wakati utajiri na kukosekana kwa usawa sasa yapo katika viwango vya juu zaidi. Miongo mingi ya kupunguzwa kwa fedha zinazotengwa kwa matumizi ya umma imewaacha mamilioni ya watu bila huduma za msingi kama vile huduma za afya, wakati juhudi za kubinafsisha huduma hizo na rasilimali (zikiwemo maji na nishati) huchangia kukosekana kwa usawa kwa sababu ya huduma za msingi kugeuzwa bidhaa zinazouzwa kulingana na sheria za soko na mahitaji ya wanahisa. Wakati huo huo, sera inayolenga kilimo cha viwandani na kilichoelekezwa nje imeshindwa kuleta usalama wa chakula hapa Afrika. Kwa kuongezea, ukosefu wa uwekezaji katika mifumo ya chakula ya mashinani ambayo husababisha uhuru wa chakula imekuwa na athari mbaya kwa viumbe na mimea, pamoja na hali ya hewa.

Vipimo vya kijinsia katika sera iliyopo bado haijatambuliwa kabisa au kuzingatiwa, pamoja na jinsi mifumo hiyo inavyochangia kukosekana kwa usawa wa kiuchumi wa wanawake kwa kunyonya kazi yao ndani na nje ya nyumba; kutoonekana, kulipwa malipo duni, kutolipwa, na ukosefu wa usalama. Wakati COVID-19 inaendelea kuzunguka bara la Afrika, kukosekana kwa nyavu za usalama wa kijamii zinazohitajika na wanawake kutokana na nafasi yao ya upungufu wa kifedha na mshtuko wa uchumi kumebaini kutofaulu kwa mfumo wa maendeleo ambao unatilia mkazo tija kwa ukuaji badala ya ustawi wa watu wa Kiafrika. Hakika COVID-19 imedhihirisha kile wanawake wamesisitiza kwa muda mrefu: kwamba faida iliyotengenezwa katika uchumi na masoko hutolewa ruzuku na utunzaji usiolipwa pamoja na kazi za nyumbani – huduma muhimu ambayo hata janga la sasa limeshindwa kukubali na kushughulikia kwa sera.

Historia inatulazimisha kutafakari sana na kwa uaminifu kuhusu athari za kuendelea kwenye njia hii ya deni. Tunatafuta fedha wakati Afrika inapeana pesa nyingi kwa dunia kuliko pesa inayopokea. Je, hii inaridhi vizazi vya baadaye ustawi? Tunajali aina na vyanzo vya fedha na masharti yanayoandamana na fedha hiyo. Katika vizazi vya nyuma, haya yameongeza mzigo wa kazi isiyolipwa kwa wanawake wa Kiafrika. Tuna tumaini na matarajio kuwa mipango yenu ya bara hili inaambatana na maono endelevu. COVID-19 imetuonyesha mahali ambapo udhaifu wetu wa muundo upo, na historia inatuonyesha kwamba njia za zamani hazifanyi kazi.

Tunatoa wito kwenu kuhakikisha kuwa mnaunda mchakato wazi na  unaojumuisha  ili kuelekeza jinsi mnavyofanya kazi na kutafsiri kile ambacho juhudi zenu za kuhamasisha msaada unazalisha. Utaratibu huu unahitaji kuenda zaidi ya kuwajumuisha ‘wataalam wa uchumi’ na pia kujumuisha vikundi ambavyo vimetengwa na mtindo wa sasa wa uchumi. Kwa kuzingatia hii, tungependa kuanza mazungumzo na nyinyi. Tunataka kusikia mawazo na maono yenu kwa nchi za Kiafrika, uchumi wa Kiafrika, uhamasishaji wa rasilimali na watu wa Kiafrika zaidi ya COVID-19. Tungependa kuwa na mkutano rasmi na nyinyi kujadili hili zaidi hata ikiwa ni kupitia wavuti. Kuna mashida zaidi yanayokuja na tunataka kuunga mkono mawazo yatakayowezesha ubunifu wa pamoja unaolengaa wakati ujao. Chini ni mapendekezo tunayotaka kuweka mbele kama hatua ya kwanza ya ushiriki wetu.

Mapendekezo:

 1. Mtambue kwamba katiba zote za Kiafrika yanahakikishia haki ya msingi ya usawa – na kwamba hii inahitaji kuunga maono na mwelekeo wa sera yoyote ikiwa ni pamoja na sera ya kiuchumi na kijamii yanayogusia COVID-19. Kwa kweli hii inamaanisha uingiliaji wa sera na mgao wa bajeti ambao unalenga kuimarisha haki kwa wale ambao wametengwa zaidi na sera za sasa na kwa hivyo kuathiriwa sana na athari za COVID-19 ikiwa ni pamoja na wanawake lakini pia inayoingiliana na upungufu wa muundo ikiwa ni pamoja na hali ya uchumi, ulemavu, hali ya virusi vya ukimwi, mwelekeo wa kijinsia na kitambulisho cha kijinsia.
 2. Mifumo ya ukuzaji na usambazaji wa chakula mashinani inapaswa kuungwa mkono na msaada wa fedha na rasilimali kwenda moja kwa moja kusaidia wakulima wadogo barani Afrika, walezi wa bioanuwai, mbegu za asili, na ardhi. Wizara za Kilimo zinapaswa kushirikiana na harakati za uchumi, hali ya hewa, na harakati ya uhuru wa chakula barani Afrika, kuachana na kilimo chenye viwandani na kuunga mkono wakulima wadogo, pamoja na haki ya wakulima ya kuhifadhi na kugawa mbegu kwa jamii, kitaifa, katika nafasi za kikanda na za Kiafrika. Kwa kuongezea, urithi wa kikoloni wa unyonyaji wa rasilimali kutoka Afrika kupitia mazoea ya kusafirisha na kuuza nje unahitaji kugeuzwa. Kwa upande wa chakula, msisitizo wa kukuza mimea chache inayouzwa katika soko za nje umepunguza tofauti wa mazao yanayofaa kwa lishe bora na lishe katika jamii zetu na imewahamisha Waafrika kutoka kwenye ardhi yao kwa kuwapa wafanyabiasahara binafsi mamilioni ya hekta za ardhi. Hii ni licha ya kujulikana kwamba ni wakulima wadogo ambao hulisha idadi kubwa ya watu barani Afrika na sio mashirika. 
 3. Mlipuko wa COVID-19 umeonyesha wazi uhusiano kati ya afya na mazingira. Kwa hivyo, kudumisha uadilifu wa mfumo wa ikolojia ya Afrika na kuwezesha jamii kupata njia za kuishi na kufaidika na mali asili inapaswa kuwa katika mpango wowote wa kufufua uchumi. Badala ya kuzingatia msingi wa soko katika uhifadhi, serikali za Kiafrika zinahitaji kuvipa kipaumbele  utunzaji na matumizi endelevu ya bianuwai kwa faida ya jamii ambazo ni walinzi wa rasilimali hiyo na ambao maisha yao yanategemea moja kwa moja rasilimali asili.
 4. Jukumu la serikali limepunguzwa mara kwa mara tangu kuanzishwa kwa mipango ya marekebisho ya kimuundo na inahitaji ujumuishaji upya, kupitia ushiriki wa moja kwa moja wa watu wa Kiafrika, ili serikali iwe mdhamini wa haki, na mpatanishi wa usambazaji wa uchumi wa kijamii na  upatikanaji sawa  wa miundombinu ya kijamii. Hii inahitaji kuwezeshwa kwa upatikanaji wa kimsingi wa ardhi, maji, chakula, huduma ya afya, elimu, nyumba, usafi wa mazingira, na teknolojia. Ushirikiano wa umma na wa kibinafsi umeficha jukumu la nchi na kuunda nafasi zisizo za kidemokrasia za ufikiaji zinazotokana na ada ya utumiaji. Kwa mfano, upatikanaji wa nishati, elimu, usafiri na afya yanashikilia wasio na kazi, tabaka la wafanyikazi na familia zinazojihusisha za kilimo serikali zinapokosa uwezo wa kutoa usaidizi unaowatosha kujikimu. 
 5. Kulingana na ILO “ajira isiyo rasmi ni chanzo kikuu cha ajira barani Afrika, na unachangia asilimia 85.8 ya ajira zote” na “karibu sekta yote ya kilimo barani Afrika ni ile isiyo rasmi [kwa asilimia 97.9].” Uchumi usio rasmi, au uchumi maarufu, ni injini ya masoko ya Afrika. Mataifa lazima yatumie fursa hii kuelekeza mifano ya kiuchumi na kinga ili kugundua kuwa misingi ya uchumi ya Kiafrika ni kazi hii isiyoonekana. Uchumi huu unachukuliwa kama ‘isiyo rasmi’ kwa sababu inaendeshwa sana na kazi ya wanawake. Vipimo kama Pato la Taifa (GNP na GDP) hazifai kwa biashara ambayo hufanyika katika sekta hii. Ipasavyo, wafanyikazi wote lazima wahakikishwe mshahara wenye heshima, kinga za usalama katika nafasi zao za kazi, na likizo ya kulipwa wanapokuwa wagonjwa
 6. Hakuna mageuzi katika utajiri wa kiuchumi na kijamii yatakayofanyika katika bara la Afrika bila kutambua thamani ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni ya uchumi wa utunzaji – ambapo utoaji wa bidhaa na huduma kwa familia na uchumi huwezeshwa kupitia kwa jasho ya wanawake wasiotajwa, wasio na malipo na wanaofanya kazi za nyumbani, na pia katika aina nyingi za sekta maarufu, kazi za wahamiaji na wa umma ambazo ni za hatari – kazi zile za mapato duni na ambazo mara nyingi hazingatii haki za wafanyikazi. Serikali imeongeza mzigo kwa wanawake kwa kuongeza utunzaji wa uzazi na kazi za nyumbani kwa sababu mara kwa mara serikali imejiondoa kutoka kwa majukumu yao ya kimataifa ya kukuza haki na usawa. Wakati wa serikali kubuni sera zinazotambua dhamana ya kazi ya utunzaji kwa mifumo ya afya na uchumi umefika, ikimaanisha serikali lazima itatoa hatua mbali mbali za usaidizi kwa sekta ya utunzaji ambayo haitegemei unyonyaji wa wanawake nyumbani na kazini. .
 7. Ni muhimu kuimarisha kipaumbele wa bajeti ya serikali katika kinga za kijamii pamoja na huduma bora za kijamii na zinazopatikana kwa watu wote. Huu ni wakati muafaka na fursa kwa mataifa ya Kiafrika sio tu kujenga uwezo wao wa kiutawala na rasilimali za kutoa huduma za kijamii, lakini pia kurejesha sifa mzuri machoni pa watu wa Kiafrika.
 8. Ni muhimu kuzingatia mikakati ambayo haishughulikii athari za moja kwa moja za COVID-19 pekee, na pia yanaimarisha upana wa mifumo ya afya na usawa katika jamii, tukikubali kuwa haya kimsingi ni mambo ya kisiasa, na kwamba yanahusu kubuni na kuhifadhi mifumo endelevu ya ustawi kwa wengi. Kumekuwa na milipuko kadhaa wa magonjwa  inayoathiri bara la Afrika katika miaka iliyopita, na COVID-19 haitakuwa ya mwisho. Kwa kweli, kukosekana kwa miundombinu ya afya na utafiti kwa magonjwa mengine kama vile ukimwi na ugonjwa wa malaria imekuwa kawaida ya kutatanisha. Kwa kuongezea, inahitajika kuelezewa wazi kuwa kupitisha kazi hii kwa wabepari ni mkakati ulioshindwa na ambayo huendeleza mtazamo kwamba serikali ya Kiafrika haiwezi kushughulikia mahitaji ya watu wa Kiafrika. Inaelekeza upendeleo zaidi kwa wabepari weupe wa kiume, ikipea fursa sauti chache za magharibi uwezo wa kusikika kuliko mataifa mengine ya Kiafrika. Nao hawana nia ya suluhisho za kimfumo kwa sababu kufikia suluhisho hizo kunahitaji kuwaondoa kutoka kwa vituo na mifumo ambayo wanaimarisha.
 9. Leseni za umiliki wa mali ya kiakili (patents) na sheria zingine husika zimeigeuza huduma ya afya barani Afrika kuwa bidhaa. Kwa kumbukumbu ya hivi karibuni, mapigano ya watu wa Kiafrika kuweza kupata matibabu ya kinga (ARV) yalichukua mamilioni ya maisha kwa sababu faida za mashirika ziliwekwa mbele kuliko maisha ya watu wa Kiafrika. Hatuwezi kuendelea kurudia makosa kama hizo daima. Ujuzi hauwezi kuwa bidhaa, na chanjo zote na dawa zinazohusiana na COVID-19 na zaidi lazima zifikishwe kwa watu wote, pamoja na maarifa yanayohusika.
 10. Zaidi ya ombi la kusitishwa kwa malipo ya deni wakati huu wa COVID-19, kufuta deni inapaswa kuwa kipaumbele. Masharti yanayozunguka misaada ya kifedha kwa bara letu pia inapaswa kukataliwa na serikali za Kiafrika. Masharti yataathiri uwezo wa nchi kupeana sera zenye kusaidia jamii kama zile zilizopendekezwa hapo juu. Pia, swala linalosisitiza maongezo ya ubinafsishaji mkubwa wa huduma muhimu (pamoja na marekebisho zaidi ya ushiriki wa sekta binafsi) yanapaswa kukosolewa na kupigwa vita na umoja wa Kiafrika.
 11. Kuongeza Uwekezaji wa nje unapaswa kuwa bila ahadi ya mapumziko ya kodi ambayo hutumika kama mwanya; kampuni nyingi za kimataifa zinazopata faida juu ya udongo wa Kiafrika zinahitaji kulipa ada zao kwa mahitaji ya watu wa Kiafrika kwanza, kabla ya wanahisa wao. Ni kwa kufuata na kutekeleza sera ya ushuru  inayolenga biashara ya kimataifa haswa ndio upungufu wa ushuru wa Afrika utashughulikiwa. Hii itakuwa muhimu kwa kuongeza mapato ya serikali za Kiafrika ikiwa uboreshaji wa kiuchumi baada ya COVID-19 utafikiwa, na kutegemea kwetu kwa deni za nje utapunguzwa.
 12. Moja kati ya msukumo wa uchumi wazi ni kuwachukulia watu wa Kiafrika kama dhamana katika michakato ya kiuchumi na mazungumzo. Mahitaji ya jamii za Kiafrika na utumiaji endelevu wa maliasili (inayohitajika zaidi katika mzozo wa hali ya hewa unaokua kwa kasi) yanaendelea kusimamishwa ili kupanga mipango ya maendeleo inayotanguliza faida ya sasa kwa gharama ya dunia na ustawi wa watu wa Kiafrika katika wakati huu na siku zijazo. Kwa sababu jamii za Kiafrika ndio walinzi wa ardhi na mazingira, jamii hizo lazima ziweze kukataa  miradi yoyote ya maendeleo inayopendekezwa. Kwa kweli, Waafrika wote wanapaswa kuelimishwa na kutoa idhini kabla ya mashauri yoyote au michakato kubwa ya sera.