Sisi,  raia na vizazi vya Afrika, kama sehemu ya Harakati za Mwamko wa Waafrika, tunachukizwa na karne nyingi za ukandamizwaji; tunalaani unyonyaji wa maliasili na rasilimali za madini na ukiukwaji wa haki zetu za binadamu.

Tunadhamiria kujenga Afrika yenye mashirikiano mapana na umoja wenye malengo ya Watu wa Afrika waliokusudia kuijenga Afrika ya Kesho tuitakayo−yenye haki ya kuishi kwa amani, yenye kuishirikisha jamii nzima na yenye kunufaika na rasilimali kwa wote.

Tarehe 23−24 Agosti 2016, wawakilishi 272 kutoka katika asasi za kijamii, vyama vya wafanyakazi, wanawake, vijana, wanaume, walemavu, wabunge, vyombo vya habari, taasisi za dini, kutoka Afrika nzima na diaspora walikutana jijini Arusha, Tanzania na kuazimia kujenga harakati za Umoja wa Waafrika unaotambua haki hizi na uhuru wa watu wetu.

 

MKUTANO UMEAZIMIA KWAMBA:

 1. Afrika ni bara tajiri. Kwamba utajiri huo ni mali ya wananchi wetu wote, sio kwa kikundi kidogo cha wanasiasa na wale wenye nguvu za kiuchumi. Ni wajibu wetu kupigania maendeleo ya kiuchumi yenye kujumuisha ushirikishwaji wa wanajamii na utunzaji wa mazingira. Tuna haki ya kuwa na maisha bora ambayo serikali zetu zimeahidi kutuletea.
 2. Waafrika wanaurithi wa tamaduni mbalimbali zenye nguvu na hadhi ya kuweza kufanikiwa kurekebisha makovu ya ubeberu wa kitamaduni katika utu na mazingira yetu. Kwa Muafrika kujipambanua na falsafa ya Ubuntu iwe ni chachu ya kujifaharisha.
 3. Tabaka la vijana wa Kiafrika ni msingi wa kujijengea ustawi katika bara letu na wanawajibika kuwa mstari wa mbele katika kujenga uamsho wa Waafrika.
 4. Waafrika waliopo katika Diaspora, wawe wale waliohamishwa kupitia mfumo wa utumwa au ukoloni au sehemu ya uhamiaji wa kipindi hiki cha sasa ni sehemu ya historia ya Afrika na ya baadaye. Ni hazina ya stadi mbalimbali, ni rasilimali na mwamko wao unatakiwa kuvunwa na kushirikishwa katika harakati zetu.
 5. Tumeazimia kupitia umiliki wa madaraka kwa wanajamii wenyewe kwa ajili ya mustakbali wa maisha yao ya baadaye, kwamba tutaunga mkono  na kushirikiana katika harakati za kijamii, kuwajengea uwezo viongozi wa vitongoji na kuzipeleka harakati zetu katika ngazi za chini ili kuzijenga harakati hizo kuanzia ngazi chini na nje ya mipaka ya jamii zetu.
 6. Tumeazimia kujenga harakati za wananchi zenye kuwajibika kwa wale waliotuchagua na kuhimiza uimarishwaji wa viwango vya juu vya uadilifu.

KWA HIYO, TUMEAMUA KUANZISHA KAMPENI KUANZIA NGAZI YA VITONGOJI, TAIFA, BARA NA ULIMWENGU MZIMA  KATIKA:

 1. Kutanua wigo wa harakati za kijamii na kisiasa.
 2. Kupigania haki ya kinamama na uhuru kwa jamii nzima.
 3. Kuelekeza jitihada zetu katika kuimarisha haki  ya usawa na heshima.
 4. Kupigania utawala bora huku tukipambana dhidi ya rushwa na vikwazo dhidi ya uwajibishwaji wa viongozi.
 5. Kupigania haki za utunzwaji wa mazingira na mabadiliko ya nchi.

WITO KWA WANANCHI WETU NA WANAHARAKATI:

Jiungeni katika hizi harakati za uamsho wa Waafrika na wahimizeni watu wetu katika dira hii ya pamoja; endesheni na ziunganisheni harakati zenu katika maeneo yenu chini ya mwamvuli  huu; jiungeni kiumoja na harakati zozote zile za Kiafrika. Misingi ya harakati hizi ni ya njia za amani. Tunasisitiza haki zetu za msingi kama Waafrika na kuzikarikibisha serikali zetu, viongozi wetu, wadau na taasisi mbalimbali kuungana nasi katika kupigania Kesho Tunayoitaka kwa ajili ya vizazi vyetu vya baadaye.

Tunadhamira ya dhati katika kuwaunganisha watu wetu wa Afrika katika kuzindua Harakati hizi ifikapo tarehe 25 Mei 2017, tutakapotanua dhana nzima ya Siku ya Ukombozi wa Mwafrika  na kutoa wito kwa sekta mbalimbali za jamii yetu katika kuwajumuisha na kuandaa tamasha  katika kila nchi ya Afrika kama sehemu ya kushamirisha ukombozi halisi wa bara letu tukufu la Afrika.